Hadithi

Umpendaye

—Hello? Hello? Vipi… Niambie!
— Yaani wewe mwenzako akikuflash huwezi kumpigia?
— Hujui yuafa, hujui kama yuaminywa!
— Aaah wacha wewe! Huna mapeni kivipi? Nyumba getikali yote hiyo ati huna za kumpigia swahiba wako simu? Mbona wapenda kujifanya wateseka hivo?
— Hahaha! Eeeeh, Usiniambie mimi.
— S’kiza basi. Nna story.
— Si umbea nawe!
— Ati? Ati napenda umbea? Ah, umbea pia lazima upewe time yake…
— Hello?
— S’kiza nikwambie basi.
— Ati wasemaje? Aaaah hii credit yako wataka tuimalize kwa salamu kumbe? Mimi mtu nakwambia nina bonge la story nataka kukupa, wewe waanza kuniuliza mambo mengine kabisa!
— Ati? Hahaha! Usinichekeshe.
— Haya basi. Ngoja basi mi pia nikuchekeshe.
— Wamwona Amina? Humjui Amina? Yaani hivi leo wewe umekuwa humjui Amina? Yaani, umehama kwenda kuishi Nyali kidogo basi inakuwa ushasahau…
— Eeeh? Sikus’kii vizuri…
— Amina, yule mtoto wa Fauzia. Eeeh Fauzia, yule mwalimu.
— Ati? Ah ah mimi sisemi huyo. Huyo ni Fauzia mwengine… sasa ubaya wako huwa hungoji mtu akamaliza kuongea. Wamkata tu!
— Ati? Haya ngoja nianze tena. Kisha ubwage sikio; unisikize kwa makini.
— Nasema Fauzia, yule ambaye yuafundisha primary kule mjini. Yule ambaye ni mweupeeee…
— Ehee, huyo huyo!
— Haya, sasa huyo Fauzia mwalimu ana mtoto yuaitwa Amina. Mtoto toto si toto. Kichuna kama nini. Akipita shingo lazima zipindwe, eh? Macho yote yamfuata yeye.
— Sasa yeye ni mtoto amemakinika sana! Mtoto na akili zake. Shuleni hana mchezo nako. Alibarikiwa na urembo na akili pia, ndo waambiwa. Alimaliza primary vizuri. Halafu, huyooo akaenda zake Nakuru, mwenyewe an’kwenda secondary.
— Haya. Akafanya mitihani yake vizuri, akapita…
— Wasemaje? Naona… Nadhani alipata B+. Nakwambia results zake zilipotokea, kulikuwa hakulaliki huku. Mtoto alinunuliwa zawadi kama nini. Akarushiwa bonge la party. Watu wa kubeba pilau manyumbani kwao walibeba; watu wa kula mpaka kushindwa kutembea wakala. Yaani, ilikuwa sherehe ya kisawasawa. Kina Diamond na Ali Kiba wakaimba Bongo Fleva mpaka asubuhi baba!
— Ati? Ebu ongea vizuri nawe. Sikuskii…
— Ah ah! Wale si Waislamu. Amina ni jina tu alipewa. Lakini wajua Amina pia si jina la Kiislamu tu. Tena hao kina Amina tangu zamani dini yao haijulikani vizuri. Ikifika Ramadhan, Fauzia yuafunga saumu; Christmas ikifika yuabandika sufuria la pilau.
— Haya. Nilikuwa nin’fika wa? Eeeh. Basi si Amina akafanyiwa party, yakaisha.
— We! Kumbe kulikuwa kuna mengine hatuyaoni. Pale kwenye karamu nas’kia kulikuja mvulana. Wala hajulikani ni mtoto wa nani.
— Nas’kia Amina alijibanza katika pembe fulani na huyo mvulana. Wenyewe walikuwa waongea sijui kizungu, sijui wasema ‘like really?’, kidogo waoneshana vitu kwa simu zao kwenye hii sijui yaitwa… yaitwaje vile? Watsa..?
— Eeeh hiyo hiyo…
— Ati? Ebu iseme tena. Watsap. Eh, hilo neno huwa lanisumbua lakini!
— Sasa, kidogo kidogo twapata habari ati Amina jamani hayuko nyumbani? Ah, ameenda wapi? Haijulikani.
— Taabu sasa. Wazungu wenyewe wasema shida bin matatizo.
— Hahahaa!
— Basi si wakujua huku mtaani? Midomo ikaanza kazi. Ooh sijui an’kwenda na yule mvulana kwao; ooh sijui amekimbia maan’ake Fauzia yuamtawisha sana. Halafu, si wawajua hawa wajinga wa huku mtaani kwetu ? Wakaanza kusemasema, “Ona sasa shida za kusomesha wasichana!”
— Basi kupeleka msichana akamaliza form four ndio imekuwa kumsomesha sana! Mbona twatia aibu watu sisi! Siku hizi watu wana madigrii matatu matatu hao wasema form four ndiyo kusomeshwa sana!
— Wacheka? Hahaha! Utacheka sana! Nakwambia nilikuwa nataka mmoja aniambie mimi hayo maneno. Nimpe lake ndio anijue, siitwi Chiriku bure.
— Ati? Ooh, eeeh! Sasa basi Fauzia maskini akawa hana imani tena. Wewe waonaje mtoto wako akipotea? Ela utalala?
— Si ndiyo? Hahaha! Hakuliki wala hakulaliki!
— Nakwambia, Fauzia akawa sasa si mwalimu tena; sasa amekuwa mtu wa kiguu na njia. Leo yuko kwa polisi, kesho yuaenda mortuary. Hali, halali mwanamke wa wenyewe.
— Sasa, siku moja mimi nilikuwa nimekwenda zangu marikiti ya kule mjini kununua viatu – si wavijua, vile vya mshipi wa nyuma.
— Ah-ah mi sisemi kama vile vyako. Mi nasema vile vya mshipi wa kupita na kisiginoni.
— Eheee! Kama vya Umi. Si wajua visigino vyangu vilivyo na aibu? Hahaha! Hivyo viatu huwa vyanisitiri aibu yangu.
— Wasemaje? Yaani hivi nisipate mume kisa ni visigino?
— Hahaha! Wacha wewe!
— Ah lakini swahibu kasha u-mbaya.
— Ati? Wajifanya hujui?
— Wewe si uliniambia dadako akitoka Dubai atarudi na mali mpya? Hivi mimi mwenzako natembea na nguo zee kambe sina anipendaye!
— Ati? Hahaha! Waona ushaanza story zako?
— Hebu kwanza lakini nikumalizie hii fununu ya Amina. Naona giza laingia na hata mchele sijaanza kudondoa. Si wamjua mamangu? We wataka aseme mpaka mate yakauke?
— Haya, sasa si mimi nilikuwa nin’kwenda zangu marikiti. Nikanunua viatu, nikaokota madera mawili pale kwa lile duka letu la Msomali. Halafu, nikaenda zangu Top Time kununua marashi.
— Sasa, wakati nageuka hivi nipande matatu ya kunirudisha nyumbani namwona msichana mweupe amejifunga hijabu an’kaa dukani, yuauza vikoi.
— Ah! Nikamwangalia vizuri. Nikasema yule si ni Amina, mtoto wa Fauzia. Nakwambia nilishangaa! Maan’ake mimi najua Amina kuzaliwa kwake kote hajawahi kuvaa hijabu lakini leo hio kavaa!
— Haya, mimi sikumzungumzia. N’kamwacha.
— Nilipofika nyumbani, hata sikuzitoa zile nguo zangu nizijaribu. Nikamketisha mamangu chini nikamweleza kila kitu. Saa tisa ya mchana hivyo. Saa kumi, saa kumi na moja hivi, mamangu akajifunga leso, akavuta mtandio wake, kisha huyo! Akaenda nyumbani kwa Fauzia.
— Hawakukaa nakwambia. Kidogo kidogo nawaona hao, wamekuja nyumbani kwetu. “Nipeleke ulikomwona Amina,” Fauzia akasema.
— Mimi nikamwambia hakuna wasiwasi, bila shaka nitampeleka. Tukalala. Kisha asubuhi yake tukaenda marikiti. Na walahi tena, tukampata.
— Eeeh, tulimpata nakwambia. Kisha, huyo Amina mwenyewe hata alipomwona mamake hakushtuka.
— Si ndiyo? Wajua alimwambia mamake vipi? Ati, “Shikamoo ma.”
— Walahi tena!
— Nakwambia mimi hata nilishangaa.
— Eh? Ngoja nitakwambia. Mbona una pupa dada?
— Fauzia akamwuliza, “Hivi wewe, umeolewa?” Amina akasema, “Eeeh ma. Hata hivi mimi unionavyo ni mjamzito.” Fauzia akasema, “Haya basi, nipeleke huko kwako nikapate kukujua.” Amina akakubali. Akafunga duka, halafu, tukaanza mwendo wa kwenda Majengo.
— Ah-ah. Majengo mpya.
— Eeh. Tulipofika basi, nakwambia kikawa kisa. Fauzia akaanza kulia kwa sauti. Sasa sisi twashangaa. Kwani amefiwa?
— Eh, dadangu. Kumbe kulikuwa na makubwa. Kumbe ule mtaa, Fauzia alikuwa yuajua vizuri sana. Alipoona ile nyumba Amina aliyoingia, akaanguka haswa.
— Mi naona hata alizirai haswa! Akaanza kusema, “Hii nyumba ni ya babako, Amina. Hii nyumba ni ya babako!”
— Ewe! Kumbe, yule mvulana wake Amina ni ndugu yake na hakuna aliyekuwa ajuaye. Basi kilio, we.
— Nakwambia. Mimi hata nikashindwa nimliwaze nani. Fauzia huku yualia; Amina huku hashikiki. Yuajitupatupa chini. Yuamtusi mamake. Fauzia mara yuamuita Mungu, mara yuamwomba Amina msamaha, mara yuatuomba sisi watu imani.
— Sa’hii? Sa’hii kumetulia. Lakini we! Nakwambia ni shida.
— Nakwambia we. Wewe ukisema una shida jua kuna wengine hata hawajui waanzie wapi.
— Eh? Ngoja nitakwambia nikipata habari zaidi. Mamangu ameenda kwa Fauzia kumwona.
— Haya, ngoja nipike huu wali. Mwambie huyo dadako anitumie madera mawili tatu, basi. Sawa?
— Haya, swahiba, bye.
— Kisha nikikuflash upige, was’kia?
— Hahaha!
— Haya, nisalimie huyo umpendaye.

Imechapishwa na Idza Luhumyo

Idza Luhumyo ni mwandishi kutoka Kenya.