Ushairi

Matiti Yangu Wapenzi

Matiti yangu, wapenzi
Vilima viwili
Mishangazo miwili
Iliyo kifuani mwangu

Matiti yangu, wapenzi
Sikuwa tayari
Kuangaliwa kiume
Sikuandaliwa

Matiti yangu, wapenzi
Mapacha mlio tofauti
Ndiyo, ninaye nimpendaye
Zaidi
Kati yenu

Matiti yangu, wapenzi
Mliulisha mwili wa mtu mwingine
Mkaupa uhai mfumo
Umeng’enyao virutubisho
Na mifumo mingine

Matiti yangu, wapenzi
Alama ya Yezebeli
Mnaoakisi mwanga
Mnaokodolewa macho na wanaume

Matiti yangu, wapenzi
Mlio bapa kifuani pangu
Mimi niliyeanzisha mapinduzi
Nanyi, mifuko miwili ya saruji
Mnaobana kifua changu
Mnaobana pumzi yangu
Wakati wanaume walipojificha kwenye siasa
Kwenye vyama na vyeo
Wakiogopa kutotaja ubini wao
Wakiogopa kusahaulika na historia

Hata hivyo,
Mimi niliwakusanya
Niliwahamasisha na kuwaelimisha
Nikawalisha yale maziwa ya kwanza ya njano
Nilizungumza kwa kifua changu
Mimi na watu wangu twataka uhuru
Mimi na watu wangu twataka kujitegemea
Mimi na watu wangu
Mimi na watu wangu

Nimetajwa kama “mengineyo” vitabuni
Maneno machache ya harakaharaka
Lakini iwekwe wazi
Taifa halikulishwa na nazi
Kifuani pangu watu walipata nguvu
Bila mimi tusingekuwa na uhuru

Maziwa yangu, wapenzi
Mnaolala kama ndala
Si chuchu saa sita tena
Hamna mvuto
Mmefika mwisho