Makala

Ninavyomkumbuka Bibi Titi

Siwezi kusahau siku niliyokutana na Bibi Titi Mohamed.

Nadhani ilikuwa mwaka 1991. Kulikuwa na sherehe ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambayo ilikuwa imeundwa na Tanganyika African National Union (TANU). Nilipewa nafasi ya kwenda kuiandikia, nikiwa mwandishi wa habari wa gazeti la serikali, Daily News.  Nilifurahi mno kupelekwa huko hasa baada ya kusikia kuwa Bibi Titi atakuwa mgeni rasmi.  Niliona raha sana kwa vile kwa mara ya kwanza nitamwona mwanamke shujaa ana kwa ana.

Kwa vile nilikuwa mwandishi wa habari niliruhusiwa kukaa kwenye viti vya mbele.  Mama Sophia Kawawa alikuwa anaongoza mkutano huo. Bibi Titi alikuwa mbele pia. Tulimpigia makofi na kumpokea kwa shangwe. Nakumbuka niliketi karibu na Bibi Titi.  Alikuwa mtu mzima, uzee umeingia, mfupi, anatembea kwa kuchechemea kwa vile mguu ulikuwa unamuuma.  Niliona kama ana unyonge fulani.

Nilibahatika kuongea na Bibi Titi, hakuwa na makuu. Nilipojitambulisha kwake, alichangamka sana na aliniambia kuwa anamfahamu baba yangu.   “Mwambie baba yako Aleck, anitafute… nataka kuongea naye.”  Nilifikisha ujumbe kwa baba. Kumbe kwenye mwaka 1966, Bibi Titi alikuwa Marekani kwa ajili ya mkutano wa akina mama.  Baba yangu wakati ule alikuwa ni mtangazaji wa Sauti ya Marekani (Voice of America) na alimhoji. Mahojano hayo  yalisikika Afrika Mashariki yote.

Hapo ndipo nilipotambua kuwa ni Bibi Titi ambaye alikuwa amenipakata nikiwa mtoto mdogo kabisa kwenye picha iliyokuwa kwenye albumu ya familia.  Na huenda ndio sababu kila mara nilitaka kujua habari zake.  Baada ya kuwaelezea watu kuhusu ile picha, wengi walikuwa wananitania kuwa ndio sababu na mimi nina kifua kikubwa.

Sikuonana naye tena baada ya ule  kwenye mkutano.  Ninasikitika kuwa sikuwaomba wakubwa zangu wa kazi ruhusa ya kwenda kufanya mahojiano naye.  Baadaye, niliskia kuwa Bibi Titi alikuwa anaumwa, na Mwalimu Nyerere alienda kumjulia hali, Halafu alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili  ya matibabu, na alifariki huko.

***

Nikiwa mtoto nakumbuka kuona picha na kusikia habari za mwanamke aliyewahi kuwa kiongozi wa kitaifa wa wanawake, Biti Titi Mohamed.  Kulikuwa na kanga zenye picha yake pia.  Nilisikia alikuwa bonge la mama kimwili, na mwenye uwezo wa kuvutia wanawake na hata wanaume akiwa jukwaani akihubiri.   Niliposikia kuwa ni Bibi Titi ndiye alikuwa anaimba ule wimbo wa ‘Hongera Mwanangu’ kwenye Radio Tanzania, niliufurahia zaidi. Lakini, kwa muda mrefu sikusikia habari zake.

Kumbe, kwa miaka kadhaa Tanzania, ilikuwa mwiko kuongea habari za  walioshiriki katika jaribio la kupindua serikali mwaka 1970 na Bibi Titi alikuwa mmoja wao.  Alikuwa amepewa kifungo cha maisha lakini alitoka gerezani baada ya kupata msamaha wa Rais mwaka 1972.  Ilikuwa ukiwauliza wakubwa habari za Bibi Titi unaambiwa nyamaza, au wanabadilisha maongezi.  Na enzi zile kulikuwa hakuna mtandao ambayo ungeweza ku-google upate habari zake.

Nikiwa nasoma A-Level Tabora Girls mwaka 1982,  mwalimu wetu wa siasa alikuwa ni mtu wa ‘chama’ hasa. Lakini alikuwa na msimamo mkali na alitaka tuelewe kuwa dunia ina mizunguzo mingi.  Aligusia habari za wanawake kwenye chama, na mimi nilimuuliza kama Bibi Titi bado yu hai.  Alisema ndiyo yu hai na anakaa Dar es Salaam.  Alituchekesha aliposema kuwa baada ya uhuru, miaka ya mwanzo  Bungeni, Bibi Titi aliwahi kusema, “We want fire in Magomeni… Fire in Small Bottles” (akimaanisha tunataka umeme Magomeni). Baada ya hapo, Mwalimu aliamua lugha rasmi ya Bunge iwe Kiswahili.

Mwalimu wetu  aliendelea kutusimulia jinsi Bibi Titi alivyokuwa waziri, na alivyokamatwa na kupelekwa kuhojiwa baada ya  jaribio la kuipindua serikali. Alisema Bibi Titi na wahaini wenzake walinyimwa chakula na maji kwa siku tatu.  Siku ya tatu, Bibi Titi alipelekwa kuonana na Mwalimu Nyerere, na kabla ya jaribio walikuwa marafiki sana. Alisema, Mwalimu Nyerere alipomuona Bibi Titi alisikitika mno na kumuuliza kwa nini alihusika.  Mwalimu alimuuliza anataka nini na Bibi Titi aliomba Coca-cola.  Waliongea, na ndipo Mwalimu aliona kuwa hao wahaini wenzake walikuwa wamempumbaza kwakuwa hakuwa msomi. Ila kwa vile alifanya kosa, ilibidi aende kukaa gerezani. Baadaye alipewa msamaha wa rais.  Mwalimu wetu aliishia hapo na hakusema zaidi juu ya Bibi Titi, ilikuwa ni siku ile tu.

Hayo ndiyo niliyoambiwa na mwalimu wangu. Baadaye nilikuja kujua kuwa japokuwa Bibi Titi alikuwa amesoma mpaka darasa la nne tu, aliweza kuwa kiongozi mzuri sana wa wanawake Tanganyika.  Akiwa TANU aliweza kuwavuta wanawake wengi kujiunga na chama cha TANU na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).  Nilijiuliza, je, angepata kisomo angeweza kufanya nini? Tukumbuke kuwa enzi zile wanawake kusoma zaidi ya shule ya msingi ilikuwa nadra.  Mwanamke kusoma mpaka darasa la nne ilikuwa bahati, na wenye bahati walifika darasa la nane.  Nafasi za kusoma sekondari zilikuwa chache na kusoma Chuo Kikuu, ilikuwa kama kushinda bahati nasibu.

Baadaye nilisikia kuwa Bibi Titi anakaa Magomeni, lakini eti ‘kajitenga’, haongei na watu, anakaa mwenyewe, watu wamemtenga, mara watu wanamwogopa, mara hivi na vile. Nadhani ilikuwa pia mwaka 1991, ambapo serikali iliamua kumtambua Bibi Titi na mchango wake katika historia ya Tanzania kwa kubadilisha jina la  Barabara ya UWT iliyopo Dar es Salaam kuwa  Barabara ya Bibi Titi Mohamed.