Umbu ni mahali ambapo wanawake wa Afrika Mashariki (na kote lugha ya Kiswahili inapotumika) watajumuika na kusimulia yaliyowakuta, mambo wanayoyawaza, yanayowakera na kuwafurahisha.
Mahali penye uhuru wa kutumia kazi za kibunifu kama mashairi na hadithi; uwanja ambao tutawaenzi mama zetu ambao historia inataka kuwasahau. Kwani imekuwepo minong’ono mingi kwenye vibaraza mbalimbali, kwamba hatuna hadithi za kutosha za wanawake wanaoandika kwa Kiswahili.
Waandishi wapo. Washairi wapo. Watunga hadithi wapo. Wapo wanawake kwenye mwambao wa Bara Hindi ambao wameacha alama kwenye maisha yetu, na kwenye ngazi ya kitaifa. Je, tutaacha sauti zao zipotee?
Umbu ni Dada. Dada yake ni bibi yako, ni mama yako, mdogo wako, mwanao, shangazi. Naye ni lazima umtunze, umuenzi, umheshimu na umpende kwa ndimi zako. Umbu ni hatua moja ya kutuleta pamoja.
Tushikane mikono, tuinuane na kupaza sauti zetu hata pale ambapo hatutakuwa na tafsiri moja ya mambo yaliyotokea. Cha msingi, tupate pa kusemea yale ya kwetu, yanayotukereketa na yanayotufurahisha.
Umbu ni sehemu ya kunakili historia, kukuza lugha ya Kiswahili na simulizi zilizoandikwa kwa jicho la mwanamke. Nasi tulikuwepo hapa. Hisia zetu, mawazo yetu na ndoto zetu zina nafasi katika dunia hii.
Mwanzilishi wa Umbu ni Esther Karin Mngodo, mtanzania mwenye mapenzi na lugha ya Kiswahili, simulizi za kubuni na wanawake wapendao hivyo pia. Umbu ni zaidi ya Bi. Mngodo. Umbu ni mimi na wewe. Karibu jamvini.