Ushairi

Titi Furaha ya Kweli

1. Titi lina miujiza nisemayo yaamini
Mwanamke hupendeza akilivaa gauni
Na mno huwapumbaza vibarobaro njiani
Titi furaha ya kweli furaha ya kila mtu

2. Titi lina maliwaza kwa mwanamume makini
‘Kilibonyeza bonyeza hujihisi yu peponi
Na pumzi humpaza akawa yu taabani
Titi furaha ya kweli furaha ya kila mtu

3. Titi lina mwangaza kwa mtoto duniani
Ndicho chakula cha kwanza atiacho mdomoni
Anyimwapo huchagiza watu hawaelewani
Titi furaha ya kweli furaha ya kila mtu

TITI LA MAMA

1. Titi la mama li tamu kushinda chochote kile
Wala haliishi hamu hata unyonye milele
Tena latia wazimu wanyonya popote pale
Mapenzi mama na mwana matiti yana mchango

2. Wanyonya huku wahema kwa utamu wa maziwa
Kukaa na kusimama na miguu kuinua
Wanyonya na kutazama sura ya mama sawia
Mapenzi mama na mwana matiti yana mchango

3. Si usiku si mchana liwe mdomoni titi
Si leo wala si jana halipitwi na wakati
Wala halina kuchina kama ‘bando’ halikati
Mapenzi mama na mwana matiti yana mchango

4. Titi halina kuchoka ukweli siyo mzaha
Hata likabwabwarika ‘kinyonya waona raha
Wanyonya huku wacheka wanachekelea siha
Raha ya titi kwa mwana si umbile ni maziwa.

Imechapishwa na Dkt. Salma Omar Hamad

Dkt. Salma Omar Hamad amezaliwa mwaka 1980 Kisiwani Pemba – Zanzibar. Kwa sasa, yeye ni muhadhiri wa Isimu na fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Kitaaluma, Dkt. Salma ana shahada ya kwanza ya Sanaa na elimu (BA ED) daraja la kwanza aliyoipata Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar mwaka 2005; somo kuu likiwa ni Kiswahili, Shahada ya umahiri katika Isimu; tahasusi ya Kiswahili aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2011 na Shahada ya uzamivu (PhD) ya Kiswahili aliyoipata Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar mwaka 2018. Katika uwanja wa fasihi ya Kiswahili; Dkt. Salma ni mwandishi chipukizi wa hadithi fupi pamoja na mashairi. Pamoja na mambo mingine, anapenda sana kusikiliza na kusimulia simulizi za aina mbalimbali, kusoma na kuandika kazi za kifashi.