Makala

Aliyoniambia Mama yangu kuhusu Bibi Titi

Bibi Titi Mohammed (1926 – 5 Novemba 2000)

Niliambiwa mengi kuhusu shujaa huyu na hayati mama yangu Bi. Fatma Kazi wa Muleba. Yeye pia alikuwa mpiganaji ambaye hakuwa na elimu ya shuleni. Binamu yake Bi. Paskazia Bwahama alikuwa mkewe Bw. John Rupia, mhimili mkuu wa Mwalimu Nyerere. Alikuwa akiongea sana na mama yangu juu ya siasa iliyokuwa imeanza kuibuka nchini ya wapigania uhuru. Ndo maana mimi nilipata picha hii ya Bibi Titi katika ujana wangu, pia  ikawa sababu mojawapo ya kuthamini uwezo wa wanawake katika nyanja nyingi. Wakati huo mimi nilikuwa nikingali mtoto.

Titi Mohamed alizaliwa jijini Dar es Salaam mnamo mwaka 1926 katika familia ya Kiislam. Wakati huo ilikuwa vigumu kupata vyeti vya kuzaliwa. Kama wenzake wengi wa wakati huo, hakupata elimu rasmi, lakini alijifunza mengi kutoka kwa wazazi wake na familia yake kwa jumla.

Bibi Titi alikuwa mwanamke mwenye kimo kifupi kama futi nne na nusu hivi, alikuwa ameumbika vizuri na amejaa katika zile sehemu zinazopendeza. Rangi yake ilikuwa kahawia kama maji ya kunde. Alikuwa na uso mpana mfupi, na macho yake yalikuwa makubwa. Alikuwa mwenye haiba ya ucheshi, ingawa alikuwa mtu mwenye msimamo na mwenye fikra ya kina.

Japokuwa hakuwa na elimu ya shuleni, alikuwa mwenye akili na mwepesi kujifunza kutoka mandhari yaliyomzunguka. Jambo hilo lilimsaidia sana kuona hali ya unyonge wa Watanganyika chini ya ukoloni. Yeye aliweza kushirikiana na watu wenye mawazo kama yake, japo walikutana kwa siri.

Mnamo miaka ya 1950, Bibi Titi alikuwa miongoni mwa wale waliopigania uhuru wa Tanganyika kutoka ukoloni wa Uingereza akiwa pamoja na Mwalimu Julius Nyerere, chini ya mwamvuli wa chama cha Tanganyika African National Union, TANU. Walikuwepo watu wengi waliotengeneza mitandao ya siri ya kukutana ili wasikamatwe na Waingereza, ambao bado walikuwa wanadharau uwezo wa Mwafrika wa kujikomboa. Mojawapo wa wapiganaji alikuwa Edward Barongo ambaye alikuwa rafiki wa familia yetu. Ingawa alikuwa akingali kijana sana, alikuwa anaitetea TANU kwa uwezo mkubwa na kwa siri. Yeye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa TANU wakati mmoja. Pia yeye alimwambia sifa za Bibi Titi na ushujaa wake.

Tanganyika ilipopata uhuru, Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyesifiwa na kupewa jina la baba wa taifa. Lakini bila ya Bibi Titi Mohamed, asingekuwa na ushawishi wa kutosha wa kufanikiwa kuikomboa nchi hiyo.

Bibi Titi alikuwa ni mwanamke wa kwanza kujiunga na harakati mbalimbali za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mwanzoni mwa harakati zake za kisiasa, alifanikiwa kulishawishi kundi kubwa la wanawake kujiunga pamoja naye. Kama kiongozi wa tawi la wanawake la chama cha TANU, alikuwa na jukumu la kuwashawishi wanawake kuunga mkono maoni na sera za TANU.

Kushuka na kupanda kwa Bibi Titi

Wengi wanajua jia la “Bibi Titi” kwasababu ya barabara maarufu jijini Dar es Salaam iliyopewa jina lake. Lakini si wengi wajuao aliyopitia mama huyu kwaajili ya nchi yetu. Barabara hii ilipewa jina lake kwa heshima ya mafaniko makubwa aliyoyafanya wakati wa mbio za kutafuta uhuru wa Mtanzania.

Baada ya uhuru wa Tanganyika na katika miaka ya mwanzo ya kuundwa kwa Tanzania, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bibi Titi alipewa uwaziri chini ya uongozi wa Rais Julius Nyerere.

Bibi Titi alikuwa mmoja wa wanawake wa kwanza mzalendo kushika nafasi za ubunge na uwaziri nchini Tanzania, (licha ya kuwa hakuwa na elimu hapo mwanzoni, aliweza kujielimisha baadaye). Lakini ghafla alipoteza cheo hicho baada ya kutokubaliana na itikadi za ujamaa za Nyerere.

Mnamo 1969, pamoja na wenzake sita, miongoni mwao Waziri wa Kazi Michael Kamaliza na maafisa wengine kadhaa wa kijeshi, Bibi Titi alikamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kupanga njama za kuipindua serikali. Bibi Titi na wenzake hao walikuwa ni watu wa kwanza nchini Tanzania kukabiliwa na mashtaka ya uhaini. Baada ya kesi kusikilizwa kwa siku 127, Bibi Mohamed alihukumiwa kifungo cha maisha.

Hata hivyo, aliachiliwa huru mnamo mwaka 1977 baada ya kusamehewa na Rais Nyerere. Baada ya hapo, aliishi maisha ya upweke bila ya familia yake wala marifiki zake aliokutana nao wakati wa harakati zake za kisiasa. Waliogopa kuwa naye, pengine wangeweza kufikiriwa vibaya.

Kupotea katika ukimya

Baada ya kutengana na Mwl. Julius Nyerere, ikawa vigumu kupata taarifa zozote zinazomhusu Bibi Titi Mohamed. Kwa muda mrefu, serikali ilikaa kimya kuhusu mchango wake na mafanikio yake.

Ukosefu huu wa kuutambua mchango wa Bibi Titi Mohamed katika harakati za ukombozi wa Tanganyika unaendana na tabia iliyozoeleka ya kutotambua michango ya wanawake, hasa ya kisiasa inayoandikwa katika vitabu vya historia.

Lakini mambo yalibadilika 1991. Katika chapisho la chama la kuadhimisha miaka 30 ya uhuru, Bibi Titi alitajwa kama “shujaa wa kike katika harakati za ukombozi”.

Yeye alifariki dunia mnamo mwaka 2000. Watanzania wengi wanamkumbuka kama ” Mama wa Taifa”

Hadi sasa Bibi Titi anaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa ushujaa wake, maisha yake, hata uasi wake ulionesha picha ya mtu ambaye alikuwa na uwezo wa kufikiri na kusema alichoamini bila kuogopa. Japokuwa alifungwa, Mw. Nyerere alilitambua hili, na alithamini utu wake.

Kwangu mimi, Bibi Titi, Bi Fatma Kazi, Bi. Paskazia Bwahama, mdogo wake Bi. Katonda Abera Bwahama, na wengine wachache walinisaidia kuwa mwanamke imara baadaye maishani, Mungu awapokee katika himaya Yake.

Laiti tungekuwa na mashujaa wengine kama hao leo, wasichana wengi wangekuwa na msimamo imara zaidi.Wao walionesha mfano kwamba wanawake wanao uwezo na wanakamilishana na wanaume, kuuwezesha ustaarabu unaoendelea daima, kusonga mbele.