Hadithi

Kafara ya Talaka

Bibi Titi aliukodolea macho mlango kwa muda mrefu baada ya mumewe kuondoka. Alipoufunga, aliufunga na ukurasa mwingine katika maisha yake na aliyekuwa mumewe. Mumewe alimwacha. Si kwa sababu alimtendea chochote wala lolote. Hakumkosea. Lakini ameachwa.

Titi alichoka tiki. Si uchovu wa mwili tu, bali pia, wa akili. Ndio ametoka Nairobi tu. Safari ya kuchosha. Alilokwenda kusuluhisha halikusuluhishwa. Amegundua, safarini alifuatwa na mtu aliyekuwa akifuata amri ya vyombo vya dola. Amerudi nyumbani akitarajia mumewe atamtuliza.

Mambo yameishia kinyume.

Amerudi nyumbani jana yake na leo yametukia haya ya kumuatua moyo.  Wamekuwa na mumewe chumbani. Mume ameondoka kwenda kuoga. Kisha naye akafuata mumewe alipomaliza. Kurudi chumbani, amempata mumewe yualia. Mwanamume ana nini? “Una nini, mume wangu? Mbona unalia?”

“Hujui nimekupa talaka leo?”

“Talaka? Talaka ya nini?”

“Nimeamua tu basi!”

“Mbona kunitaliki? Nimefanya nini mimi? Nimefanya dhambi gani sasa? Ulijua nilikwenda Nairobi na kwa nini nikaenda. Wala sikukaa hata siku tatu! Tunazozania nini mume wangu? Kwamba nimejiuzulu?”

“Waliniambia nisingepata kazi maana una nyumba nyingi za kukodisha! Utaweza kukubali nikikwambia uziuze?”

“Hivi huoni tulipaswa kujadili haya kabla ya kunipakaza talaka nisiyoilalia wala kuiamkia?”

“Nakuacha ufanye utakayo. Kwa heri.” Baada ya kutamka haya, mtu mume akaondoka.

Mawazo yalimzonga Titi. Hajafanya kosa lolote. Basi, mbona atalikiwe? Hii ndoa ya pili, imekwenda tu. Angalau ya awali, alijua mumewe alishachoshwa na uanaharakati wake. Lakini hii, hapakuwepo dalili yoyote. Imelipuka tu, bila taarifa.

Hakupata japo lepe la usingizi usiku huu ambao mumewe aliamua kumuacha. Aliyaona maisha yake ya ndoa yakimpitikia machoni. Tangu ile ya utotoni.

Alikumbuka akiwa mwali wa miaka kumi na minne. Kaozwa mume, jibaba la miaka arobaini. Hawakuwa na maneno ya kuwaunganisha. Titi bado mtoto na michezo yake. Huyu mtu mzima na mambo yake ya utu uzima. Titi hakufahamu mizungu ya ndoa na mzee Haji hakuwa tayari kuwa mwalimu. Ya nini ajisumbue na tayari kuna waliofuzu? Hajuti kuolewa na mzee yule. Alimpata bintiye Halima. Binti ambaye, alihakikisha amesoma akizingatia yeye hakusoma sana. Masomo kwanza, ndoa baadaye. Alhamdullilahi!

Mume wa pili alikuwa mume. Kama ndoa hufungwa mbinguni, basi hii ilifungiwa kule kwa hakika. Si mapenzi hayo aliyopata kutoka kwa mumewe. Buku bin Athmani alikuwa karani mkuu katika Idara ya Usambazaji Maji. Alikuwa mume miongoni mwa waume. Alipoaga dunia, Titi alipatwa na kihoro kwa muda. Aah, uhai hutoa Mwenyezi Mungu, akautwaa atakapo!

Titi alijishughulisha na uimbaji wake. Mwimbaji mkuu wa kikundi cha Roho ni Mgeni. Mahiri wa kutunga nyimbo na kuongoza uimbaji katika ngoma. Alijitosa uwanjani kuficha maumivu yake; uimbaji ukamponya.

Hakuchagua siasa. Zilimpata ametulia nyumbani tu. Shemeji yake, Sheneda alikuwa keshawatajia kuhusu TANU, hata akawaletea yeye na mumewe kadi za chama. Akawafahamisha kuhusu kijana kwa jina Nyerere aliyekuwa amejitosa ulingoni kupigania uhuru wa nchi yake. Alipomkumbuka huyu ‘kijana’, Titi alishusha pumzi. Kweli dunia duara. Mambo yaweza kupinduka kichwamgomba. Ivushayo ikawa mbovu.

Kisha akaja yule mzungu, Hatch. Alikuwa ameona utitiri wa watu. Walikuwapo hata wanawake katika umati ule wa takribani watu elfu ishirini. Naye akataka kujua, “Vipi, mna tawi la wanawake katika chama chenu? Au wao huja tu wakasikiliza, kisha wakaenda zao?”

“Wapo, bila shaka,” viongozi wa TANU walimjibu bila kusita.

“Basi naomba kukutana nao.”

Duh! Walikuwa wamejifunga kwa ndimi zao. Hawakuwa na viongozi wa kike maana wanawake walipaswa kukaa nyumbani, chini ya himaya ya waume zao. Wangefanya nini na tayari washamwahidi Hatch? Sheneda akapendekeza suluhu.

“Nitakwenda kumchukua Titi. Atatutoa katika shimo hili tulilojichimbia.”

“Haa! Lakini Titi ni mke wa watu!”

“Mumewe ni rafiki yangu. Nitazungumza naye, atamruhusu Titi kuja.” Hawakutaka kumvunja moyo. Lakini, ukweli hawakuamini mume yeyote angemruhusu mkewe kuhusika. Maana, hata wao hawakutaka wake zao kushiriki.

Sheneda alimwendea Boi, mumewe Titi. Akamweleza ahadi waliyompa Hatch. Akamwomba amruhusu mkewe kukutana na huyu bwana mzungu. Titi alishangaa ghaya kwa jibu la mumewe. “Mchukueni, yupo hapa. Utamjia saa ngapi?”

Titi hakuulizwa maoni yake.

“Nitakuja kumchukua saa tisa, maana Hatch yuaja saa kumi.”

Titi akamwambia Sheneda amwendee na jamaa yake Tatu binti Mzee waandamane naye. Hivyo ndivyo, mumewe alivyomruhusu kutia guu siasani.

Hakujua ya baadaye.

Siasa zilimpokea Titi kwa mikono miwili. Akaupata umaarufu. Kila mara safarini kote nchini kuwahimiza wanawake kushiriki shughuli za chama na hivyo kupigania uhuru wa nchi yao. Hotuba zake zilivutia. Wanawake waliutii wito wake. Wakajazana mikutanoni. Wakajiunga na chama kwa wingi.

Titi hakutulia nyumbani. Angekuwa safarini kwa miezi mitatu. Akirudi nyumbani, baada ya siku kama kumi hivi, anaingia katika safari nyingine. Juhudi za kuunganisha nchi nzima hazikuwa rahisi na Titi alijitoa mhanga.

Kawaida ya binadamu, hawakosi la kuamba. Wanawake walioshiriki katika juhudi za TANU na safari hizi nyingi wakapata kibandiko chenye jina ‘malaya’. Titi na wenzake hawakujali sana. Waliamini watu wakishaona matokeo wataacha kuwasingizia.

Hatimaye, Boi akachoshwa na hizo safari za mkewe. Alijuta kumpa ruhusa kujitosa katika siasa. Akamwambia Titi, alikusudia kumwoa mke wa pili. Titi hakujali. Alimwambia aoe lakini amwache aendelee na kazi zake za kisiasa. Boi alioa mke wa pili. Jina lake Khadija. Lakini, hawakupatana na hatimaye akamtaliki.

Siku moja, wakati Titi akijiandaa kwa safari yake nyingine, Boi akamwambia hakutaka kuoa tena.“Nataka mke wangu, tuishi kama zamani. Uache hizo safari zako. Ukae nyumbani kama wake wengine kama unanipenda.”

“Mume wangu mpenzi, wewe wajua hii kazi siwezi kuiacha. Uhuru ni muhimu na kuna watu chungu wananitegemea. Nishakwambia, kama wataka kuoa mke mwengine, oa tafadhali! Ila niache niendelee na kazi zangu.”

“Mmmmh, nikuache wasema, sio? Basi nitakuacha!”

Titi hakuitilia maanani kauli yake Boi. Hakutaka kuzuiwa kusafiri. Si kampa yeye ruhusa hapo mwanzo? Kwa vile Boi alikuwa dereva wa teksi, Titi alipata nafasi ya kupanga safari yake, wala hakumwambia mumewe. Aliuficha mkoba wake nyumbani kwa mdogo wake wa kike. Hivyo, Boi hakuwa na taarifa kuhusu mpango wa mkewe kusafiri kesho yake. Titi alifyata ulimi. Tayari, Boi alishakwenda kuteta kwa viongozi wa chama, kwamba kilimpoka mkewe. Mmoja wa viongozi wa chama akamwambia Titi asisafiri kama hakuwa na radhi ya mumewe. Titi akamkumbusha kuwa, mumewe ndiye aliyetoa idhini mwanzoni.

Boi alifika kwenye kituo cha garimoshi na kupata kuwa, mkewe alikuwa keshaabiri, tayari kwa safari. Kulikuwepo watu waliofika kumuaga Titi. Boi hakupata nafasi ya kusema na mkewe.

Titi alikuwa mjini Mwanza alipopata barua ya mwanawe akisema babake aliacha barua na kuondoka nyumbani. Titi hakuamini hadi aliporudi nyumbani na kupata talaka imemsubiri. Alitalikiwa kwa juhudi zake za kupigania uhuru wa nchi yake.

Na leo hii tena, miaka kumi baadaye, mume wake mwingine amemtaliki. Kwa sababu, yeye sasa anachukuliwa kuwa adui wa serikali ambayo aliipigania. Amejitolea sabili kuhakikisha nchi yake imepata uhuru na sasa uhuru huo ndio unamhangaisha.

Aliukumbuka ushauri wa Kambona, “Watakutia ndani, Bibi Titi. Kimbia.”

“Siwezi. Mamangu mzee atakufa kwa kihoro. Nimejiuzulu. Sijaiba. Sijanyang’anya. Sijatenda kosa lolote. Wakitaka kunitia mbaroni, na waje. Nimejitoa mhanga kwa ajili ya nchi hii. Ikiwa wanataka uhai wangu, na wachukue.”

Walishaichukua ndoa yake tayari.

Bibi Titi alizusha pumzi. Usiku wa manane sasa. Akaamka na kuingia msalani. Kisha, akaingia kitandani kusubiri yale ambayo mapambazuko yangemletea.

MWISHO

Imechapishwa na Rachel Maina

Bi. Rachel Maina ni mwalimu wa Kiswahili mwenye tajriba ya miaka mingi. Ana shahada ya uzamili katika Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi, Kenya. Amefunza Kiswahili katika viwango mbalimbali nchini Kenya na Marekani. Baina ya 2018 na 2021, alifunza Kiswahili katika Chuo Kikuu cha St. Lawrence, New York, Marekani. Hivi sasa ni mwanafunzi wa uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison ambapo pia anafunza Kiswahili. Kadhalika, Bi. Maina hujishughulisha na masuala ya utafiti wa lugha, fasihi na uana. Amewasilisha tafiti zake katika makongamano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Kadhalika, ameandika kazi za ziada kwa wanafunzi wa shule za upili, pamoja na hadithi fupi ambazo zimechapishwa katika mikusanyiko mbalimbali. Anajishughulisha pia katika tafsiri za Kiswahili-Kiingereza na Kiingereza-Kiswahili.