Makala

Nguvu ya Matiti

Huwa ninawaza, ni nini haswa kinawafanya watu wawe wanahaha wakiona matiti ya mwanamke? Je, ni weusi wa chuchu zake? Au ni umbile la titi lenyewe? Ni huku kuhaha kunakofanya mwanamke anapokiuka utaratibu wa kujifunika kuwe na nguvu, na haswa kisiasa.

Ndiyo, mwili wa mwanamke kama binadamu yeyote yule umeumbwa kwa ajili ya matumizi binafsi. Lakini Bistoria* (neno ambalo nimelitunga mwenyewe kumaanisha simulizi za binadamu) mbalimbali zinaonesha kuwa binadamu wa kale kwenye maeneo mengi yasiyo na baridi kali waliishi bila kujifunika sana miili yao. Tunaambiwa kwamba pamoja na kuishi maisha yanayoweza kwa sasa kuitwa maisha ya ‘uchi’ hakuna ushahidi wowote kwamba mashambulio ya mwili yalikuwa mengi kwa wanawake kama tunavyoona sasa hivi kwenye mifumo ambayo tunavaa nguo.

Inabidi tufahamu kuwa kuna tofauti kati ya uchi na utupu. Wakati utupu (nudity) ni mwili ambao haujafunikwa kabisa kwa chochote na zaidi viungo vinavyoitwa vya siri kuwa wazi, uchi (nakedness) imekuwa inatafsiriwa kama mwili ulioachwa wazi kwa sehemu kubwa.

Jamii nyingi za kiafrika nazo kupitia ukoloni na zaidi umisionari wa Kikristu zilianza kuona kana kwamba kutokuvaa nguo ni ‘dhambi’. Kuna tetesi kwamba wakoloni na wamisionari wengi kwa vile walitokea nchi za baridi, kwao kujifunika (kuvaa nguo) ulikuwa ni utamaduni wao tofauti na nchi nyingi za Afrika ambazo hali ya hewa ni joto.

Sasa tuko kwenye wakati ambao kuvaa nguo ni utamaduni uliozoeleka. Na zaidi ni wakati ambapo mwanamke tofauti na mwanaume anategemewa kuhakikisha mwili wake wote hasa maeneo ambayo kwa jicho la ‘kiume’ yanapandisha ashki yamefunikwa. Maeneo hayo ni makalio, matiti, uke na maeneo mengine hata makwapa na mapaja wakati mwingine yanaonekana kama sehemu ya uchi wa mwanamke.

Sasa basi, nini kitatokea iwapo mwanamke ataamua kuacha mwili wake uchi? Nadharia zinatuongoza kuona kuwa pamoja na madhila yote ya mfumodume na mifumo mingine ya ugandamizaji na uonevu dhidi ya mwanamke. Adhabu mbaya kwa mifumo hii ya kikatili ni kwa mwanamke kutembea uchi kama njia ya kupinga dhana au jambo fulani. Kwa maana nyingine mwanamke anapoamua kufunua kile mfumo unamlazimisha afunike, ni ushujaa na ushindi dhidi ya wanaoeneza ubaya.

Hivyo upingaji wa kutumia uchi ni moja ya nguzo muhimu za kuhakikisha wanawake wanapata haki au dhamana wanayostahili kwenye mfumo usiowapa fursa ya kupata haki hizo. Kumekuwa na matukio ya kibistoria yenye kuonesha joto la vuguvugu la ukombozi kupitia mwili wa mwanamke. Moja ya kumbukumbu za siku za hivi karibuni kwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda Dkt. Stella Nyanzi ambae alifanya upingaji wa kutumia uchi dhidi ya uonevu na unyanyasaji dhidi ya mkuu wake wa kazi Profesa Mahmood Mamdani.

Ingawa kitendo cha Stella Nyanzi kilitafsiriwa kwa namna mbalimbali bado ninaona wazi kuwa hoja ya Stella ni kuhakikisha mfumo ambao umekuwa na tabia ya kumdharau mwanamake kwa sababu ana uke wake (ikimaanisha viungo vyake vinamuainisha mwanamke kama matiti na uke wenyewe) unaatingishwa.

Kwa wale wanawake ambao wanafanya upingaji wa utupu huenda mbali zaidi kuhakikusha madai yao yanasikilizwa. Mara nyingi wanawake hawa huonesha uke au matiti yao kama silaha pekee ambayo wanayo katika kudai kile wanachokitaka. Njia hii huumiza sana wale waumini wa mfumodume kwani mfumodume mara nyingi umeonesha uke na matumizi yake ni kwa ajili ya mwanaume. Hali hii imelazimisha watu wengine kuamini kuwa mwanaume ndiye mwenye hatimiliki za uke wa mwanamke. Kutokana na mfumo kulazimisha haya, mwanamke mara nyingi ananyang’anywa umiliki wa mwili wake mwenyewe.

Kuna wengine wanaodai kuwa wananawake wanaotumia uchi au utupu kwenye kupinga jambo fulani wanafanya hivyo ili vyombo vya habari viwaone (seeking attention). Ukweli ni kuwa hilo ndilo muhimu, kwamba naonesha mwili wangu hadharani ili vyombo vya habari viweze kusaidia kuhabarisha kuhusu jambo langu ninalolitaka liwafikie watu wengi zaidi.

Kuna kundi jingine ambalo linaona vitendo vya kupinga kwa kutumia uchi au utupu si ‘utamaduni’ wa Waafrika, ni mambo ambayo ya yanafanyika kwenye nchi za Ulaya na Amerika. Ukweli ni kwamba masuala haya wa wanawake kutumia miili yao kupinga jambo fulani yana mizizi yake barani Afrika. Utaona kwamba, pamoja na ukweli kwamba Dkt.Nyanzi alifanya kitendo hicho cha upingaji wa kutumia uchi, si mwanamke wa kwanza kufanya hivyo.

Wanawake wa Igbo walimpinga mkoloni wa Kiingereza kwa sheria ngumu za kodi katika kile kinachojulikana kama “Vita vya Wanawake” vya 1929” (ilipo Nigeria ya sasa). Wanawake hao walipinga kuwepo kwa mahakama ya kikoloni, na kudai kuwa wanawake nao wahudumu kwenye mahakama hizo. Pia walitaka angalau mwanamke mmoja awe Mkuu wa Wilaya. Walitaka wazungu wote waondoke! Madai yao yote yalikataliwa.

Kwahiyo, walimpinga mkoloni kwa kile kilichokuwa kinajulikana kama “Kumkalia Mwanaume” kimila, ambapo wanawake wangeenda nyumbani kwa mwanaume ambaye  amemkosea mwanamke mwenzao au kawavunjia heshima wao kama kundi. Hapo wangecheza na kuimba nyimbo za kejeli, walitaka kujua kama yeye ni mwanamume kweli.

Kuvua nguo nako kulikuwepo kwenye tukio hilo walipokuwa wanampinga mkoloni. Hii ilikuwa zaidi ya kutumia mkuki au sime. Miili yao ilikuwa silaha.

Zaidi ya wanawake wa Igbo, Pauline Opango, mke wa Patrice Lumumba aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 1961 alifanya upingaji wa kutumia uchi mjini Leopoldville (sasa Kinshasa) na kuelekea makao makuu ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Kibelgiji uliomuua mume wake kikatili. Dhihaka waliyopata wakoloni na watawala wa Kibelgiji ndio hivyo hivyo wa utawala wa Chuo Kikuu cha Makerere wamejikuta wakidhihakiwa na Dkt. Nyanzi. Na ndivyo ilivyokuwa mwaka 1992 ambapo wamama walivua nguo hadharani mjini Nairobi wakidai kuachiliwa kwa wana wao waliokuwa wafungwa wa kisiasa. Mmojawapo kati yao alikuwa mshindi wa tuzo ya Nobel Wangari Maathai.

Hivyo mwanamke ambaye kwa msingi wa malezi, makuzi na mazingira ya kisheria na kiimani ameaminishwa kutofunika mwili wake sasa anapoamua kuweka uanauke wake hadharani ni wazi kuwa anatumia silaha yake ya mwisho katika kubomoa mifumo gandamizi na ya kinyonyaji. Kwa mantiki hiyo katika vita ya haki, mwili wa mwanamke ukiwa uchi hadharani ni silaha ya hatari zaidi kuliko vifaru, mabomu na risasi. Na kwa kuwa wanyanyasaji wengi huona mwili wa mwanamke kama chombo cha starehe, wanapokiona kimesimama mbele yao, hufadhaika zaidi na mara nyingi kukimbilia kuwafunika wanawake wanaofanya hayo. Uzuri wakati zoezi la kufunika linafanyika, ujumbe unakuwa umeshafika.