Ushairi

Nibatize

“Nahitaji moto,
Nahitaji moto kwenye vichupa vidogo vidogo”

Nibatize Titi

“Nahitaji moto,
Nahitaji moto kwenye vichupa vidogo vidogo”

Kwenye mto wa kale uliokauka
Nivishe kaniki, na kibwebwe cha mcheza ngoma
Mikuki ya shaba nigawe kwa yote kaya

Nibatize mwaka 1955
Ambapo meza ziligeuka kuwa ardhi
Ndimi zangu kamba, za kuvuta wengi wafuasi
Kete nikazirusha kwa wamama na mabinti
Nibaki chachu japo sitakua nikiishi

Nibatize jioni
Jiko likihisi upweke wangu
Matandabui yakitambaa, kutawanya mashuka tangu
Masafaa ya gari moshi kuoana na nafsi yangu
Kutwa kutafuta uhuru wangu

Nibatize Titi
Nibatize mwaka 1955
Nibatize jioni
Nilie chini ya sanamu ya mkoloni
Nikichana pindo za sketi zenye hadithi ya firauni

Nibatize
Nibatize
Niwashe moto kwenye vichupa vidogo vidogo
Nibatize
Nibatize leo

Peponi
Mwili huwezi kulala wima
Mwili wangu hujikunja
Huvaa umbo la nusu mduara
Kila nikikulisha
Kama vile unataka kukuzunguka
Kama vile unakulinda

Mwili wangu huwezi simama wima
Kichwa chako kipumzikapo kifuani
Huinama kama kijakazi kwa mfalme
Kama vile kukuvuta
Kama vile kukusikilizisha muziki unaotunza

Njoo lala kifuani kwangu
Kibanda cha roho yangu
Mzizi wa mti unachanua kwa mwanangu
Njoo lala kifuani kwangu
Njoo lala peponi

SAUTI
Nasikia sauti katikati ya ukuta
Nasikia vishindo vya wacheza ngoma
Mipasuko kwenye ardhi
Ngurumo ya radi

Nasikia sauti iliyokuzwa
Nasikia misuguano ya satini ya magauni
Minon’gono inayobadilika kuwa kelele
Hatua za kujisogeza mbele

Nasikia sauti ya mikutano
Nasikia jogoo wakiwika wika
Hatua za mkoloni akikimbia
Pilau likianza kunukia

Nasikia sauti
Nasikia sauti yangu
Kama pepo pembezoni mwa bahari
Kama mwangaza wa jua usoni
Kama mbegu iliyozikwa ikachanua
Kama nanga, msingi wa majira yetu
Msingi wa uhuru.