Makala

Matiti, Uwanja wa Mapambano

Matiti ya mwanamke, kama vile ulivyo mwili wake wote, ni uwanja wa mapambano. Wakati naandika kitabu cha ‘Mektildis Kapinga: A Silent Hero’, ambacho pia kimetafsiriwa na Elias Mutani kwa lugha ya Kiswahili kama ‘Mektildis Kapinga: Shujaa Mkimya’, kinachohusu maisha ya Mektildis – mwanamke, mwalimu, mama, na mwanajeshi shupavu wa maisha aliyepigana vita kali dhidi ya saratani kwa miaka 12 – kuna maswali mengi nilijiuliza, na niliyomuuliza yeye. Lakini sikuweza hata mara moja kumuuliza aliishije bila matiti yake ambayo yalikatwa kwa sababu ya saratani.

Siyo kwamba sikutaka kumuuliza, bali sikuweza. Uzito wa nafsi ya mtu anayepigania uhai wake kwa udi na uvumba ulinielemea. Kuishi, kusalimika, kujisalimisha, imani, nguvu na matumaini ndio dhima zilizotawala mazungumzo yetu. Kwakweli niliogopa kumuuliza kuhusu kifo – kama alikua tayari kufa, au alikiogopa. Nakumbuka siku ile ya kwanza niliyoanza kumuhoji. Dera lake la njano lililokuwa na maua ya zambarau, lilishuka kifuani kwake bila ya kupinda. Kifua chake kilibaki bapa baada ya kukatwa matiti yake yote mawili. Lakini mbele ya macho yangu, muonekano wa kifua chake haukua na utofauti wa kipekee na makovu mengine yalioenea mwilini mwake — malengelenge yaliyochomoza shingoni mwake, ukakamavu wa shingo yake, ule weusi tii uliotanda kwenye viganja na nyayo zake zilivyobadilika rangi kutokana na tiba-kemikali, jinsi macho yake yaliyofifia uangavu, na kichwa chake kilivyopoteza nywele zote.

Mektildis ni mmoja wa wahanga wa ugonjwa wa saratani unaoendelea kushambulia na hata kutuondolea wapendwa wetu siku hadi siku. Lakini, kikubwa alichokitambua Mektildis kuanzia mwanzo wa kuugua kwake ni kuwa saratani sio kifo. Aliamua kupambana vilivyo, liwalo na liwe, hata kukatwa matiti. Na hata hivi sasa ninapoandika, wapo wapambanaji wengi wenye mtazamo kama wake.

Nina rafiki yangu ambaye juzijuzi tu ametoka kumaliza tiba-mionzi na tiba-kemikali baada ya kukatwa  ziwa moja ili kuokoa maisha yake.  Rafiki yangu bado mdogo sana, miaka thelathini na kidogo tu. Bado dunia na familia yake vinamuhitaji sana. Tena ni mrembo haswa asiyekaukiwa tabasamu na macho angavu yaliyojaa ujasiri.  Na kuanzia atambuzi wa ugonjwa hadi leo hii, amepambana na bado anaendelea kupambana kitemi, kwa nguvu zake zote na sala zake zote. Pamoja na hofu na maumivu anayoyapitia, huamka alfajiri na kupanda daladala kwenda hadi Ocean Road kutibiwa. Jioni, hurudi nyumbani, tena peke yake, ili aishi na aendelee kulea watoto wake wawili. Nikimfikiria, na nikijiweka kwenye viatu vyake, mwili wote unasisimka. Najiuliza, ujasiri wote huu ametoa wapi? Ulikuwepo ndani yake siku zote hizi au ameuchota kutoka kisima fulani ambacho mwenyezi Mungu amemuonesha? Lakini, hata mara moja, siwezi  kuhoji ni nini kimetokea kwenye uanamke wake baada ya kukatwa ziwa.  Siwezi!

Naelewa kuwa wengi wanaamini kuwa alama ya mwanamke ipo kwenye matiti yake, au nyonga, au kizazi. Najua tuliambiwa kuwa mabadiliko yale wakati tunavunja ungo – unyororo wa sauti na ngozi, kupanuka kwa nyonga na kuota matiti ndio haswa zilikua alama kuwa tunakuwa wanawake. Tena nina rafiki yangu mwingine ambaye tukiwa shule ya msingi, alitamani sana kuota matiti mapema kiasi cha kuweka fukufuku kwenye kifua chake ili wamng’ate, avimbe, aonekane kama na yeye ameota vipera vya matiti yale ya kwanza. Sitakuwa mkweli nikisema kua sijawahi kuliwazia hata dakika moja swali hili. Kwani na mimi naishi dunia hii hii ambayo hutuangalia wanawake kwa maumbile yetu, na kutuaminisha kuwa thamani yetu inatokana na muonekano wetu kuwa wa namna fulani. Tena, katika kila nafasi, tunakumbushwa kuwa sisi si zaidi ya maumbile. Matiti. Nyonga. Kizazi. Miguu.

Ingawa sikumuuliza Mektildis, naamini kabisa kuna sekunde kadhaa katika safari yake ambapo alifikiria juu ya kifua chake, japo kwa mbali. Pengine alikwazwa na kuchukizwa na mabadiliko yake, pengine aliwaza kama mume wake alimtazama na kumpenda kama zamani. Naamini pia, kuna watu wananilaumu kwa nini sikumuuliza alijisikiaje kuhusu muonekano wake, kuhusu uanamke wake, kama ukosefu wa matiti ulimtatiza na kumnyima usingizi. Lakini halinisumbui hilo.

Kuna wakati huwa nafikiria, labda matiti ni uhai. Siku ya kwanza mtoto akizaliwa, baada ya kulia, kikubwa kinachotarajiwa ni yeye kufanikiwa kukamata chuchu kwa midomo yake na kunyonya. Mama hufanya chochote kumpatia mtoto wake maziwa. Lakini mara anaposhindwa, hutafuta njia mbadala. Kazi ya mama haswa inakua siyo kumnyonyesha tu mtoto, bali kuhakikisha mtoto anasalimika na kuishi. Kama mama ana matatizo, au pengine anaishi na virusi vya ukimwi, basi kumpa mtoto uhai siyo kumpa titi, bali ni kumnyima titi. Hivyo, hata kama ukiyachukulia matiti kuwa alama ya uhai, kamwe hayawezi kuzidi uhai wenyewe. Kwa Mektildis, na wahanga wengine wa saratani ya titi, alama ya utu wao ipo kwenye ujasiri, imani, nguvu na matumaini yao katika kujiokoa na ugonjwa huo. Makovu kwenye vifua vyao ni alama moja tu ya ujasiri wao.

Kwenye mazungumzo yetu yote, Mektildis alikua ni mtu aliyejaa shukrani kwa Mola wake, kwa kumnusuru na kumbakisha na watoto wake. Maana siku ya kwanza alipopata majibu ya vipimo yaliyoonyesha kuwa ana ugonjwa wa saratani, mtoto wake mdogo ndio kwanza alikua darasa la kwanza. Na kukatwa kwake titi la kwanza, na baadae titi la pili, kulimkopesha miaka 12 ya kuishi na mpenzi wake, kulea watoto wake, kuuguza na hatimaye kuzika wazazi wake, kusoma, kupanda cheo kazini, kuona watoto wake wakihitimu na kushirikiana na wanajamii wenzake kwenye mambo mbali mbali.

Hakunitamkia hata siku moja kuwa alikua mnyonge au alijiona amepungukiwa na kitu. Kwake, makovu yake yalikua ni baraka na kudra. Mektildis alinionesha kuwa, kama mtu ana nia thabiti ya kuishi na kuendelea kuwepo duniani kwa ajili ya watoto wake kama alivyokuwa Mektildis, hatakuwa tayari kupoteza kiungo kimoja au viwili kwa ajili ya uhai anaoutamani. Na ninaamini pia, ujasiri wake ulimuongezea haiba yake kwa wapendwa wake, kwani ingawa hakuna anayejua kesho yake, kwenye ugonjwa kama saratani, thamani ya leo na thamani ya wakati huongezeka maradufu. Ni nani mwenye akili timamu atakuwa radhi kupoteza wakati wa kupenda kisa mpendwa wake ana makovu?

Baada ya kuandika kitabu hiki cha Mektildis, mwanamke aliyekatwa matiti kujiokoa na saratani, maswali pekee yaliyobaki akilini mwangu ni haya: kuwa mwanamke kwenye dunia ya leo, ni nini kama siyo kuwa jasiri, kuwa jemedari, kuwa mtu anayejisalimisha ili jamii isalimike? Bila mwanamke, dunia ni nini kama si tambara bovu tu? Na hadi sasa, sijutii kutokumuuliza Mektildis juu ya kuishi bila matiti yake. Hata nikipata nafasi tena ya kuzungumza nae leo, sitamuuliza. Kwani nimejua kwa hakika, kwa mashujaa kama Mektildis – matiti ni uwanja mwingine tu wa mapambano unaodhihirisha ujasiri wa mwanamke kukabili changamoto zozote zinazomkumba. Maana, nusra ya mwanamke ni nusra ya jamii yake yote.

Imechapishwa na Neema Komba

Neema Komba ni mshairi na mwandishi kutoka Tanzania. Ni mtunzi wa vitabu vya Mektildis Kapinga: a silent hero (Mektildis Kapinga: shujaa mkimya) na Diwani ya mashairi ya ‘See Through the Complicated’. Pia ni mwandishi wa insha ya “The Search for Magical Mbuji” kwenye mkusanyiko wa masimulizi ya nathari kutoka Afrika ‘Safe House: Explorations in Creative Nonfiction’. Kazi zake nyingine za ushairi, fasihi na nathari zinapatikana kwenye machapisho kama Payback and Other Stories: An anthology for African and African Diaspora Short Stories, Adda Stories, Index on censorship, This is Africa na Vijana FM. Ni mshindi wa tuzo ya fasihi ya Etisalat kwenye kipengele cha hadithi fupi sana (flash fiction) kwa mwaka 2014. Hadithi yake ya Let them eat fruit cake iliyochapishwa kwenye jarida la Index on Censorship ilitajwa kwenye orodha ya tuzo za Stack kama utunzi bora wa hadithi kwa mwaka 2019. Neema pia ni mwanzilishi mwenza wa La Poetista, iliyojikita na uandaaji wa maonyesho ya ughani wa mashairi. Kupitia La Poetista, aliandaa maonyesho ya kimataifa ya ushairi ya Woman Scream nchini Tanzania kwa ajili ya kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake mesks 3013-2015, na pia amekua mshauri na mkufunzi wa masuala ya fasihi hasa kwa waandishi chupukizi. Neema amewahi kuwa jaji kwenye mashindano ya hadithi fupi ya Andika na Soma, na Project Sawti Poetry Prize, pia ni mshauri wa kamati ya Tuzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein. Neema ni mwanachama wa UWASHATA (Umoja wa Washairi Tanzania) na Writers Space Africa -Tanzania. Mbali na shughuli za fasihi, Neema ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Amimeita Ventures Limited inayojikita na utengenezaji wa mafuta ya asili ya mbu (Ira repel) nchini Tanzania. Hujitolea kwenye mashirika ya kijamii ya TETEA, Ambitious Tanzania na RAMWI-Tampa. Pia ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Uchumi cha Hanken kilichopo Ufini.