Musa na Hamis ni majirani walioshibana haswa. Urafiki wao unajulikana na kila mtu wa kijijini kwao huko Viroja.
Marafiki hawa wote ni wavuvi. Kutokana na urafiki wao, wake zao pia, imewalazimu kuwa marafiki. Aisha au Mama Zulfa ni mke wa Musa. Rukia au Mama Zuwena ni mke wa Hamis. Urafiki ukaendelea. Halafu, ukaendelezwa na watoto wao Zulfa na Zuwena.
Yote niliyokueleza hapo mwanzo si hadithi. Wala, si jambo la ajabu kusikia kuhusu urafiki na marafiki. Ni kweli. Lakini, katika urafiki huu kuna cha ziada ambacho ndicho hasa nataka kukusimulia.
Musa alipomwoa Aisha alikuwa na matarajio makubwa sana juu ya ndoa yake na maisha yake. Baada ya mwaka mmoja tu wa ndoa yao, walijaaliwa kupata mtoto wa kiume. Wakamwita Ahmed. Ahmed alikuwa mtoto mwenye afya nzuri. Lakini, baada ya miezi mitatu tu, alifariki. Aisha na Musa walifadhaika sana. Wakajipa moyo kwa kusema, “Kazi ya Mungu haina makosa.”
Baada ya miaka miwili, Aisha na Musa wakapata tena mtoto wa kiume. Mtoto huyo wakamwita Mwinshehe. Mwinshehe alikuwa na afya nzuri na alifanana na baba yake. Miezi mitatu ikapita, mtoto Mwinshehe naye akafa. Huzuni ya Aisha na Musa haikuwa na mfano.
“Lazima kuna mkono wa mtu,” Aisha na Musa walisema.
Waliamua kuhama eneo lile. Waliwaza, ‘Lazima kutakuwa na wanga na vigagula wanaoroga watoto wa wenzao.’
Hapo ndipo, walipohamia mji wa Viroja. Walipofika huko, walikutana na jirani zao ambao ni Hamis na mkewe, Rukia. Walifurahi na kusema, “Afadhali tumehamia huku. Tumekutana na watu wema na wakarimu.”
Haikuchukua muda, Aisha akawa mjamzito kwa mara ya tatu. Miezi tisa ilipotimia alijifungua mtoto wa kike. Binti mrembo kama mama yake. Furaha ya Musa na Aisha haikuwa na kifani. Walimpa binti yao jina la Haijat. Haijat hakuwa na kasoro. Alikuwa na afya tele.
Baada ya miezi mitatu, mtoto Haijat alifariki.
“Hee! Jamani! Hii sasa imezidi. Mkosi gani huu?’ Aisha na Musa walilia huku wakiwa wamekata tamaa. Majirani zao Hamisi na Rukia walifika kuwafariji. Aisha na Musa walisimulia madhila mengine ya kufiwa na watoto wawili wa kiume hapo kabla. Rukia na Hamisi waliwasikiliza kwa makini.
Siku zilipita na majonzi yaliongezeka.
“Hawa wachawi jamani, hawataki kutuachia? Tumehama mtaa, bado wamtufuata hadi huku?” Aisha alilia kwa huzuni kila siku, akiilaumu bahati yake mbaya.
Rukia alimtembelea Aisha mara kwa mara na kumfariji. Rukia ni mwanamke mwenye maarifa mengi sana. Maarifa haya ameyarithi kwa marehemu bibi yake aliyekuwa mtaalamu wa tiba asili.
Rukia alikuwa na shauku ya kujua sababu hasa ya watoto wa Aisha kufariki baada ya kuzaliwa, tena wakiwa na umri uleule wa miezi mitatu? Alianza kufanya utafiti. Kuna watu wengine wakisikia utafiti wanawaza mbali kweli. Wanafikiri kufanya utafiti lazima uwe na shahada au stashahada. Si kweli, mtu yeyote anaweza kefanya utafiti.
Utafiti wa Aisha ulimwelekeza kuwa, kuna baadhi ya wanawake ambao kwa sababu fulani matiti yao hutoa maziwa yenye sumu. Wanawake hao, wakiwanyonyesha watoto wao, yale maziwa huwaua watoto. Haya ndiyo maajabu ya Bwana Rajabu kuzaa mtoto kumwita Mwajabu.
Rukia alimfuata Aisha na kumweleza juu ya matokeo ya utafiti wake.
“Shoga’angu inawezekana una tatizo hilo,” Rukia alimwambia Aisha.
“Nitafanyaje sasa? Maana, hapa tayari nina ujauzito wa miezi miwili,” Aisha alisema kwa sauti ya mashaka na hofu.
Rukia akamwambia, “Usijali, hata mimi nina ujauzito wa miezi miwili. Tutajifungua wakati mmoja. Hivyo, nitakunyonyeshea mwanao.”
Aisha hakuamini alichokisia. Lakini, atafanyaje? Anamtaka mtoto kwa moyo wake wote. Ndoa za Kiafrika bila mtoto ni mashaka, hivyo alikubali.
Urafiki wa Aisha na Rukia ukanoga. Mimba zao zikakua. Kila walipoyaangalia matumbo yao yaliyofutuka, waliangua kicheko. Miezi ikapita. Rukia alikuwa wa kwanza kujifungua mtoto wa kike. Akamwita Zuwena. Baada ya siku mbili, Aisha naye akajifungua mtoto wa kike. Akamwita Zulfa.
Kazi ikaanza. Kwa usiri mkubwa, Rukia aliwanyonyesha watoto wote wawili. Miezi ikapita. Watoto walipokaribia miezi mitatu, Aisha alikuwa na mashaka. Lakini, miezi mitatu ikapita, na minne na mwaka. Zuwena na Zulfa wakawa kama mapacha, wakaendelea kukua wakiwa na furaha tele.
Musa alikuwa na furaha sana kwa mtoto wao huyu kunusurika. Kamwe hakujua, kulikuwa na siri ya titi la jirani.