Hadithi

Kidonda

Shani Kijaki alisimama kwa hamaki, mkononi angali ameishikilia simu ya mumewe kwa ghadhabu. Kila alichokiona na kukisoma kilimwongezea jazba. Ilimtembea kifuani mwake, mithili ya mawimbi ya maji katika bahari iliyochafuka.

Hakuweza kufanya staamala. Alikuja kutanabahi tayari amekwishaibamiza simu kwenye sakafu. Vipande vyake vilitawanyika huku na kule utadhani nyumba iliyosambazwa na tetemeko la ardhi.

Baada ya muda, aliinama na kuokota kipande cha simu ile. Akachomoa kadi ya simu, kisha akakibamiza tena sakafuni. Mikono yake iliendelea kutetemeka, ilhali kijasho chembamba kikimchuruzika kwenye paji la uso. Papi za mdomo zilimcheza kama mtoto anayetaka kujifunza kuongea. Mashavu yake manene na meupe, yalitengeneza misingi kwa mbali, kila alipoubetuwa mdomo wake.

Kuyenga Shamu aliinuka toka kitandani. Akasimama sakafuni akiwa ametahayari. Hulka yake ya unyamavu na uraufu vilimfanya aonekane dhaifu, tofauti kabisa na mwonekano wake wa ushupavu uliochagizwa na ukubwa wa umbile lake, mithili ya Lebron James – yule mcheza kikapu mashuhuri duniani.

Kuyenga aliganda kwa sekunde kadhaa akimtazama mkewe – na asijue la kufanya. Kwa fadhaa, aliinama sakafuni na kuvikusanya vipande vya simu yake. Kisha, alikwenda kuvitia ndani ya begi lake dogo, alilokuwa amelitundika kwenye msumari nyuma ya mlango.

Kila hatua aliyoipiga Kuyenga, Shani alimgeukia akiwa amejiandaa kumrukia wapigane. Kwa bahati, hakudiriki hata kumgusa.

Badala yake, aliishika simu yake na kuufungua ujumbe aliojitumia kutoka kwenye simu ya mumewe. Akausoma kwa sauti iliyojaa kitetemeshi cha hasira:

Ile sidiria imenikaa vizuri sana. Natamani ungeniona, una macho ya kupima kifua. Bado naikumbuka mikono yako uliponifunga kwa nyuma.

Alipousoma ujumbe ule, Shani alirudi kitandani. Akavuta shuka kwa nguvu na kujifunika gubigubi. Mtoto wake mchanga wa miezi sita alilia kwa sauti kubwa kana kwamba alishuhudia tafrani iliyotandani chumbani.

****

Hekaheka na purukushani za soko la Mchikichini, Karume, jijini Dar es Salaam, zilivuma kwa mzizimo wa aina yake. Wafanyabiashara walishindana kunadi bidhaa zao kwa sauti kubwa; wengine wakitumia midomo na wengine wakitumia spika maalumu. Na wapo ambao walitumia nyimbo mbalimbali, wakichagiza kwa kupiga makofi kukamata nadhari za wateja katika biashara zao.

Wapo waliowakaribisha wateja kwa lugha za staha; na wapo waliokosa maadili ya kibiashara kwa kuwavuta wateja mabega na mikono, kuwavutia kwenye meza kununua bidhaa zao. Makundi ya watu yalipishana huku na kule. Vibaka nao hawakuwa nyuma, walitanda nyuma ya meza mbalimbali za biashara zilizozungukwa na wateja.

Kuyenga, almaarufu kama ‘Kei Masidiria’ alijizolea umaarufu mkubwa katika sokoni hapo. Wateja wake hawakuwa na kazi kubwa ya kuchagua sidiria kila walipofika mezani kwake. Ilichukua nusu dakika tu, kwa Kuyenga kumtazama mteja wake kifuani, na kujua ukubwa wa sidiria imfaayo.

 Mezani kwa Kuyenga kulisheheni sidiria ariari, kwa ubora na ukubwa tofauti. Hakuna aliyeondoka mezani kwake bila kupata ya kipimo chake; iwe mwenye madogo mithili ya embe sindano, makubwa mithili mapapai, yaliyolala mithili ya kandambili, na hata yale maarufu kama ‘saa sita’.

Gharama za sidiria zilipishana. Na zilipangwa kwa kadri ya ubora. Zilizotundikwa juu ukutani, zilitofautiana bei na zile zilizomwagwa mezani. Zilizotundikwa juu, na bei yake ilikuwa juu. Vivyo hivyo, bei ya chini kwa zilizomwaga kwenye meza ya chini. Kwa umahiri huo, ni mteja gani wa bidhaa hizo, angeshindwa kumfahamu Kei Masidiria? Labda, kwa mgeni wa mji aliyeshushwa siku hiyo na garimoshi.

Mbali na ubora wa bidhaa na umahiri wake wa kutambua hitaji la mteja, ucheshi na uchangamfu wake kwa wateja viliyakoleza mafanikio yake. Pamoja na haiba yake ya unyamavu, lakini bado hakuishiwa maneno matamu ya ushawishi kwa wateja.

Kwa kila aliyemjua fika Kuyenga, bila shaka aliigundua tofauti siku hiyo. Muda mwingi alionekana kuzama kwenye dimbwi la mawazo. Ule ucheshi wake kwa wateja uliibuka na kutoweka kama homa ya masaa. Siku hiyo, aliketi kwenye stuli pembezoni mwa meza yake. Mara kadhaa aliivua baraghashia yake, akajikuna kipara chake kilichong’aa kwa mafuta aliyojipaka.

Kimwili alikuwa hapo sokoni. Lakini kihisia, alisafiri masafa marefu hadi nyumbani kwake, Buza Kanisani, alikoacha mke na mtoto mchanga. Utamu wa biashara yake kwa wingi wa wateja mezani kwake, haukuweza kupooza ladha ya uchungu kichwani mwake. Kila alipochotwa na kumbukumbu ya mgogoro wake na mkewe, unaoelekea kuteteresha ndoa yao.

“Muuzaji yuko wapi?” alisaili dada mmoja aliyekuwa akijaribisha sidiria. Akaangaza huku na kule.

“Nipo hapa dada,” Kuyenga alijibu akijiinua toka kwenye stuli, na kumsogelea mteja. “Karibu, karibu!”

“Vipi hii, imenikaa vizuri?” dada yule aliuliza huku akijiangalia kwenye kioo. “Ila huku nyuma sijaweza kuifunga, hebu unisaidie.”

Alijigeuza na kumpa mgongo Kuyenga.

Japo macho ya Kuyenga yalijielekeza kwenye sidiria tu, lakini hakuachia kutupia jicho maeneo mengine katika umbile la mteja wake. Na hapo ndipo, aliposhuhudia kiuno chembamba mithili ya nyigu kilivyojibandika juu ya makalio manene ya mduara.  Skin tight ya rangi udhurungi ilimchora vizuri, ilhali blauzi yake nyeusi ikiruhusu sehemu kubwa ya maungo yake kutathminika.

Bila kusema lolote, Kuyenga alikwenda ukutani akatungua sidiria nyingine, na kumpatia mteja huyo. “Jaribu kuangalia na hii.”

“Lakini mimi nimeipenda hii,” dada yule alisema akiendelea kujitazama kwenye kioo, huku akiyashika maziwa yake na kuyapeleka huku na kule, kuona kama ilimkaa vyema. Kupitia kioo, Kuyenga akayagongesha machoye na mteja.

“Hiyo nd’o maana unashindwa kuifunga, siyo size yako.”

“Acha ubishi basi kaka,” dada alisema kwa sauti ya utulivu huku akijaribu kujifunga kwa nyuma yeye mwenyewe. “Nimekwambia unisaidie kunifunga, lakini naona unatatarika maneno tu.”

Kuyenga akazunguka nyuma yake ili amsaidie kumfunga, lakini kabla hajamgusa, akawa tayari amefanikiwa kujifunga mwenyewe. Akajifaragua kusema, “Naona hata hii imekukaa poa tu. Kama vipi chukua hii hii.”

“Naweza kukulipa kwa kutumia simu?” dada yule alihoji akitia nguo yake kwenye mfuko.

“Hapana, sina simu. Nenda tu kibanda cha pale mbele ukatoe.” Alinyoosha mkono akimwelekeza.

“Unaishije bila simu mjini hapa? Unayafanya maisha kuwa magumu,” alisema akielekea kibandani.

Si punde, alirejea na kulipia.

Kuyenga alirudi kuketi wakati wateja wengine wakiendelea kuchagua sidiria.

Wateja walipopungua, akakimbilia maduka ya Kariakoo na kununua simu ndogo. Haikuwa na laini.

 Akawaza, hii nayo itavunjwa tu. Simu tatu sasa zimevunjwa.

****

Majira ya saa kumi na mbili jioni, Kuyenga alifunga biashara yake na kurejea nyumbani. Kutokana na adha za usafiri, alifika nyumbani usiku ukiwa umekwishaingia. Aliingia nyumbani kwake kama mfungwa anayepelekwa Kondem kunyongwa. Alijawa wahka wa kutaka kujua endapo kadhi ya jana yake usiku ilipita kimyakimya, au la. Ukimya ulihanikiza nyumba nzima. Giza mfano wa lile la ndani ya tumbo la chewa, lilitanda vyumba vyote.

          Ishara ya kwanza kwamba mkewe hakuwemo ndani ilimcharaza.

Haraka, aliangalia ufunguo juu ya mlango, ambapo huzificha mmoja wao anapotoka, hakuziona. Uso ukamshuka. Uchovu wa kazi ukaongezewa na uchovu wa sononeko. Akarudi hatua mbili nyuma na kujongea mlangoni kwa mmoja kati ya wapangaji wenziye.

“Mama Koku,” Kuyenga aliita huku akigonga mlango. “Mama Koku!”

“Aah, taratibu basi… kugonga gani mlango kama ugomvi,” Mama Koku alisikika akilalama kutokea ndani.

“Habari za jioni Mama Koku?” Kuyenga alitoa salamu akiwa bado amesimama mlangoni. “Mimi Kuyenga.”

“Ooh jirani, karibu,” Mama Koku alisema huku akifungua mlango na kutoka.

Alijifunga khanga mbili; moja ikianzia kiuoni kwenda chini, na nyingine ikianzia chini ya makwapa. Nywele zake alizosuka ‘tatu-kichwa’ zilifumuka ovyovyo kama mchicha ulioparuriwa na kuku.

“Ahsante jirani. Kumradhi kukufunguza usiku usiku.”

“Hata nilikuwa nimelala basi? Niko macho tu nayatafakari ya dunia,” Mama Koku alisema. “Haya kulikoni?”

“Samahani, sijamkuta mke wangu, na hata funguo hajaacha. Amekwenda wapi?”

“Ukisikia maajabu nd’o haya,” Mama Koku alijibu huku akifanya kuegemea mlangoni. “Ikiwa wewe unayempa kula, hujui mkeo alipo, miye n’tajuaje?”

“Hakukuaga?”

Mama Koku akabetua mdomo akisema, “Kama hakukuaga wewe unayempetipeti usiku, ataniaga mimi wa kushinda naye nusu ya mchana tu?”

Kuyenga alipiga kimya. Akameza funda la mate hadi koromeo lake likacheza ukuti. Alificha ghadhabu yake moyoni na kusema, “Mama Koku acha basi majibu mkato. Nimekuuliza kwa sababu wewe ni swahiba wake. Ikiwa hadi imemlazimu kuondoka na mtoto mdogo, na asiache hata funguo, bila shaka alikuaga!”

Mama Koku alimtazama Kuyenga huku tabasamu lake likichanganyika na fadhaa usoni.

Baada ya kutazamana kwa muda mfupi mfano wa majogoo yanayojiandaa kurukiana, akasema, “Hivi nyie wanaume mnataka nini haswa? Kwa nini hamridhiki? Kabinti karembo, kamekuletea na mtoto mzuri mashaallah; kujifungua tu, tayari unamwona kama gunia la viazi mbatata! Kwa nini lakini?”

“Najua amekusimulia alichohisi, lakini ukweli hauko hivyo,” Kuyenga alisema kwa kitete. “Hebu tuyaache hayo kwa sasa, tafadhali kama unajua alipo naomba uniambie – usiku huu asijekupata taabu na mtoto.”

“Ungekuwa unayajua hayo, wala usingevurugwa akili na matiti ya wanunuzi wa hizo sidiria zako, hadi mnapeana na namba za simu!” alijibu huku akifuatisha na msonyo. “Mimi sijui alipo. Labda ukajaribu kumwangalia kwa wakwe zako.”

Kuyenga hakusubiri kuendelea kusomewa risala ndefu kama utenzi wa mashairi. Akageuza, na kuanza kupuyanga; mguu mosi – mguu pili akielekea kwa wakweze. Saa nne kasoro usiku, ilimkuta huko.

“Shikamoo mama,” Kuyenga alisalimia baada ya kuketi sebuleni.

“Marahaba. Hamjambo?”

Neno ‘hamjambo’ lilimgutusha Kuyenga. Alishindwa kujua ajibu ‘Sijambo’ au ‘Hatujambo’. Atajibuje ‘Sijambo’ ilhali ameulizwa ‘Hamjambo’? Na, atajibuje ‘Hatujambo’ hali ya kuwa hajui mahala alipo mkewe? Akabaki amebung’aa macho.

“Aah Mungu ni mwema mama, alimradi tunapumua. Sijui ninyi hapa nyumbani!”

“Sisi hatujambo kabisa,” mama Shani alijibu kwa utulivu pasi na papara.

“Mama uniwie radhi kukuvamieni usiku,” Kuyenga alisema huku akitafuta maneno ya kufungulia mjadala. “Nimekuja kumwangalia Shani kama yupo huku?”

“Sijakuelewa bado!” mama Shani alijibu kwa mshangao.

Kuyenga alijikohoza kidogo ili kutengeza sauti, ndipo akasema, “Nimerudi nyumbani usiku huu, sijamkuta. Majirani nao hawajui alikokwenda. Ndipo nikaja hapa.”

“Simu yake umeipiga?”

“Hapana mama, sijampigia.”

Mama Shani alichukua simu yake iliyokuwa kwenye mkono wa kochi. Alibofya vitufe vya namba, akaiweka sikioni.

Kuyenga aliganda akimtazama mkwewe, moyoni akimwomba Mungu Shani apokee simu.

“Haipokelewi,” mama Shani aliitoa simu sikioni na kumtazama Kuyenga usoni. “Kwani kumetokea nini?”

Kuyenga hakujibu. Alipiga kimya kana kwamba hakusikia alichoulizwa. Akili yake ilimpaa kwa mawazo. Aliwaza, kama kwa mama yake hayupo, hapana shaka Mama Koku anajua alipo. Atanieleza alipo.

Alitoka kwa kasi bila kumuaga mkwewe. Alidhamiria kwenda moja kwa moja kwa Mama Koku kumwangushia timbwili la nguvu. Alipoikaribia nyumba yao, akastaajabu kuona mwanga wa taa ukiwa umeenea vyumbani.

Nani amewasha taa ilhali Shani hayupo? Alijiuliza huku akijongea kwa taharuki.

Alijitoma ndani kwa pupa. Aliangaza sebuleni, hakumwona. Alipoingia chumbani, akamkuta mtoto kitandani, lakini Shani hayupo. Aliganda kwa muda bila kujua amguse mtoto, au atoke kwenda kumtafuta mkewe nje.

Akiwa bado anachanganua hoja kichwani mwake, alisikia sauti za nyayo zikitokea sebuleni. Haraka akatoka kuchungulia. Akakutana na mkewe akitokea uwani, akiwa amejitanda kanga moja na kopo la maji, huku mguu mmoja akichechemea.

“Ulikwenda wapi?” Kuyenga alimsaili mkewe.

Shani hakujibu.

“Na huo mguu umefanyaje?” Kuyenga alirusha swali lingine.

Shani alimtazama Kuyenga mithili ya paka aliyeingiza mzoga ndani.

***

Kelele za mtoto akilia, ndizo zilimshitua Kuyenga usingizini. Alijivuta kwenye kochi na kujinyoosha viungo hadi vikaachia mlio kama wa mbao zinazovunjika. Miale ya jua ilipenya kupitia kwenye matundu ya mabati chakavu. Alisimama na kuingia chumbani.

Alimkuta Shani ameketi kitandani huku akimnyonyesha mtoto.

“Umeamkaje mpenzi?” Kuyenga alimsabahi mkewe huku amesimama pembeni yake.

Hakujibiwa.

“Shani, hebu niambie, unataka niache hii biashara?” Kuyenga aliuliza kwa upole huku akienda kuketi kitandani – karibu na Shani.

Shani aliinuka kitandani na kwenda kuketi kwenye kigoda kilichokuwa pembeni.

“Shani,” Kuyenga aliita. “Kwa nini unafanya hivyo? Hivi nami nikikunyamazia kutakalika kweli humu ndani?”

“Kwani umelazimishwa kunisemesha?” hatimaye, Shani alijibu.

“Tazama, umeshavunja simu zangu tatu mpaka sasa, tutaendelea kweli?” Kuyenga aliinuka kitandani na kumsogelea pale alipoketi. “Kama hutaki nifanye hii biashara niambie tu.”

“Wewe uache biashara ya kushikashika matiti ya wanawake?” Shani alisonya.

“Suala si kushika matiti ya mtu yeyote. Ile ni biashara ya kutuingizia riziki yetu.”

“Riziki ya kupitia kwenye titi la mtu mpaka unasifiwa kwa macho ya kupima kifua na mikono ya kuwafunga vizuri? Riziki gani hiyo?”

Kuyenga alimsogelea Shani na kuchuchumaa karibu yake. Akamwekea mkono begani.

“Usinishike,” Shani alibwata huku akimtoa Kuyenga mkono begani kwake, almanusura ya kumwangusha mtoto.

Papo hapo walisikia mlango wao ukigongwa.

Kuyenga alimtazama Shani, lakini Shani hakushughulishwa na huyo agongaye mlango.

Mlango uligongwa kwa mara ya pili.

“Karibu,” Kuyenga alisema na kuinuka.

Alipokwenda kufungua mlango, alikuta uso kwa uso na Mama Shani pamoja na shangaziye Shani.

“Ooh, mama,” Kuyenga alijifaragua kuwalaki kwa furaha huku akiificha aibu yake moyoni. “Karibuni ndani.”

“Ahsante baba!”

Waliingia na kwenda kuketi kwenye kochi dogo la watu wawili.

Kuyenga naye aliketi kwenye kochi dogo la mtu mmoja.

 “Haya habari za nyumbani?” Kuyenga alianzisha mazungumzo.

“Habari ni mbaya,” mama Shani alijibu. “Unajua kabisa jana umekuja na taarifa mbaya nyumbani kwangu, na kama haitoshi ukaondoka ghafla ghafla tu. Lakini juu ya yote hayo, umekaa kimya bila kunijuza kilichojiri… ulitegemeaje?”

Shani alitoka chumbani baada ya kusikia sauti ya mama yake. Hakutarajia.

“Enhee, kulikoni?” mama mkwe alihoji akiwatazama.

“Mama naomba umuulize mwanao mwenyewe,” Kuyenga alimtazama Shani ambaye alikaa kwenye stuli kulia kwake baada ya kutoa salamu.

Shani alitulia mithili ya tui la kwanza kwenye bakuli. Alihisi chumvi imezidi mboga. Alihisi kuumia kwake kulisababishwa na mahaba yaliyopitiliza kwa mumewe.

“Mimi simwelewi mume wangu, tabia zake zimekuwa mwiba mkali kwenye hii ndoa.”

“Hebu fafanua vizuri?” shangazi yake alisema.

“Ni zaidi ya mara tano nimeona meseji kwenye simu ya mme wangu. Zote zikihusisha wanawake.”

Shani aliusoma ujumbe wa mara ya mwisho kuingia simu ya mumewe.

Ile sidiria imenikaa vizuri sana. Natamani ungeniona, una macho ya kupima kifua. Bado naikumbuka mikono yako uliponifunga kwa nyuma.

“Biashara nd’o inaleta yote haya mama. Hao ni wateja tu. Wanawake wengine wapo hivyo, wanapenda kuchombeza. Na nikisema nisiwape namba za simu, nitapoteza wateja. Mke wangu anayajua haya yote. Na anajua jinsi navyofanya biashara. Huu ni wivu tu ambao mpaka sasa, ameshavunja simu zangu tatu,” Kuyenga alitoa maelezo yaliyoonekana ni utetezi.

“Penye wengi hapahariki neno. Leo tutachimba msingi na kuezeka kabisa. Madhali hili swala lipo kwetu, kila kitu kitakwenda sawa,” shangazi alimwambia Shani aliyekuwa akilia.

          “Mama, shangazi,” Kuyenga aliita. Akaongea kwa utulivu akimtazama mkewe. “Mke wangu mimi, nilimpatia huko huko kwenye biashara. Alikuwa anaona jinsi ninavyochangamana na wanawake. Apunguze wivu tu. Ninampenda mke wangu, sijawahi kumkosea adabu.”

Wote walikuwa tuli. Kuyenga akaendelea, “Nakiri udhaifu wa kutoa namba ya simu. Lakini, siyo kwa dhumuni baya, mke wangu. Ni kwa ajili ya biashara tu. Sitatoa wala kupokea namba ya simu. Nitawapa namba ya mke wangu.”

Kwa kauli ya mwisho ya Kuyenga, wote wakaangukua kicheko, kasoro Shani.

Kikao kikahitimishwa kwa kuombana radhi. Shani aliahidi kupunguza tabia ya wivu kwa mumewe, Kuyenga akaahidi kutoitoa namba ya simu kwa wateja wake.

Si punde, mlango uligongwa. Kuyenga akaufungua.

 “Naitwa Koplo Getrude Funuka, kutoka kituo cha polisi Buza.” Alionesha kitambulisho chake.

“Hatujaita askari sisi lakini,” Kuyenga alisema kwa tashwishwi.

Kuyenga aliwakaribisha ndani, askari polisi na dada aliyefuatana na afande.

Shani aliweka mkono usoni kujiziba. Alipomwona yule dada mwenye POP alizidi kuingiwa na hofu. Hakutulia kama kipa anayezuia penati. Si hai si maiti kwa kihoro.

“Ni huyu hapa afande,” yule dada aliulekeza mkono kwa Shani.

“Kwani kuna nini?” Mama yake Shani alihoji.

“Huyu dada ni mwendawazimu alinipiga hadi kunivunja mkono, akidai nina mahusiano ya kimapemzi na mumewe.”

Baada ya ule ugomvi, Shani aliwasiliana na dada aliyetuma ujumbe usiku kwenye simu ya mumewe. Akamlaghai ana mzigo mpya atamwuzia kwa punguzo kubwa, hivyo waonane. Dada bila kujua, akaingia kumi na nane za Shani, kwa kujua ni Kuyenga.

Siku ambayo mumewe alirudi nyumbani na kutomkuta, ndio siku Shani aliyopigana hadi kuchechemea. 

“Mama nisaidie.” Akamsogelea mama yake ambaye hakuelewa nini cha kufanya kwa muda huo.

Machozi yalimtiririka hadi usawa wa kidevu. Mwili wake ulizizima.

“Mwanangu analia sasa nani atambembeleza na kumnyonyesha?” Shani alisema na kumtazama mumewe baada ya kusikia sauti ya kilio cha mtoto ikitokea chumbani.

          Alihisi kidonda cha wivu kinakwenda kumlaza korokoroni.

Imechapishwa na Lilian Mbaga

Lilian Mbaga ni mwandishi wa vitabu vya Riwaya na vitabu vya Hadithi za wototo. Vitabu vya Riwaya: Tabasamu la Uchungu (2014), Hatinafsi (2018) Tuzo (2019) kitabu kilichoandikwa kwa ushirikiano wa waandishi watano. Vitabu vya watoto: Paka na Juli, Simba muoga, Kisa cha Samaki kuishi majini, Sara na Paulo katika msitu wa ajabu. Pia, Lilian ni mwanachama wa chama cha Waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI).