na Esther Karin Mngodo
Watu wengi wanamfahamu Bibi Titi Mohamed kama mwanamke aliyefanya “kitu fulani” kihistoria nchini Tanzania. Lakini alifanya nini? Ana mchango gani? Nini kilimpata? Ni miaka 21 sasa tangu atutoke. Lakini ni nadra kumsikia vinywani mwa watu. Ukweli ni kwamba, bila yeye na wanawake wengine waliokuwa hai wakati wa harakati za kupigania uhuru, mambo mengi yangekwama.
Titi ni mkusanyiko wa hadithi, mashairi na makala ambayo yanamsheherehekea Bibi Titi. Lakini pia, katika kucheza na maneno, Titi ni kiungo katika mwili wa mwanadamu lenye utashi wake. Kiungo hiki mwilini mwa mwanamke kina mambo yake ambayo yanamtofautisha mwanamke kwa uzuri, majukumu ya kuwa mama, na kadhalika.
Waandishi wa hadithi katika jarida hili la kwanza ni pamoja na Lilian Mbaga, Rachel Maina, Isabela Lucas, na Idza Luhumyo. Waandishi wa mashairi ni Ngollo Mlengenya, Manka John, na Dk Salma Omar Hamad. Makala zimeandikwa na Dk Vicensia Shule, Neema Komba, Sally Qazi na Chemi Che-Mponda.
Nawashukuru wahariri waliofanyia kazi jarida hili, Elizabeth Mahenge, Fadhy Mtanga, Fausta Musokwa, Nancy Lazaro, Neema Komba. Shukurani za pekee zimwendee Dk. Chambi Chachage kwa mchango wake katika kufanikisha jarida hili.
Ahsante sana Dinah Manongi aliyechora michoro iliyotumika, Upendo Mchome aliyetengeneza tovuti ya Umbu na kusimamia uwasilishaji wa kiubunifu kwa kushirikiana na Frank Ntevi.
Karibu jamvini, tusome Titi.
Karibuni Umbu.